Saturday, July 31, 2010
   
Text Size

Tafuta kwenye Website hii

Maalim Seif aendelea kupumzishwa zaidi hospitalini

HALI ya katibu mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad inaendelea vizuri, lakini bado hajaruhusiwa kutoka hospitalini na watu hawaruhusiwi kumuona kwa kile kilichoelezwa na msaidizi wake, Jussa Ismail Jussa kuwa ni kumpa muda wa kupumzika na kuwa karibu na daktari.

Maalim Seif amelazwa Hospitali ya Hindu Mandal iliyo jijini Dar es Salaam tangu Ijumaa baada ya kuugua ghafla ugonjwa wa mkamba (bronchitis), ambao hutokana na kuvimba kwa njia za hewa, baada ya mapafu kushambuliwa na vijidudu.

Alikumbwa na ugonjwa huo akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere akisubiri kupanda ndege ambayo ingempeleka Muscat, Oman.

Juzi mganga wa mwanasiasa huyo, Dk Kaushik Ramaiya alisema kuwa hali ya Maalim Seif ilikuwa inaendelea vizuri na kwamba angeruhusiwa kuondoka hospitalini jana tofauti ya matarajio ya awali ambayo yalikuwa siku nne.

Lakini jana, baada ya Mwananchi kufika hospitalini hapo saa 4:00 asubuhi na kukutana na mganga wake, Dk Kaushik Ramaiya, ilielezwa kuwa kiongozi huyo wa upinzani visiwani Zanzibar ataendelea kuwa hospitalini hapo.

Dk Kaushik, hata hivyo, alieleza kuwa hali ya Maalim Seif inaendelea vizuri, lakini bado wanaendelea kumuangalia hadi kesho (leo).

"Bado hatujamruhusu, tumemshauri aendelee kupumzika lakini anaendelea vizuri sana," alisema Dk Kaushik.

Alifafanua kuwa Maalim Seif huenda akaruhusiwa kuanzia leo, kwa kuwa hali yake imeendelea kuimarika kutokana na vipimo na dawa alizopata hospitalini hapo.

Naye msaidizi wake wa karibu, Ismail Jussa, ambaye pia ni mbunge wa kuteuliwa wa CUF na msaidizi wa karibu wa Maalim Seif, ilielezwa kuwa mwanasiasa huyo ataendelea kuwa hospitalini hapo licha ya hali yake kuendelea kutengemaa.

Jussa alisema hali ya Maalim Seif inaendelea vizuri na kwamba hawatamruhusu mwandishi yeyote kuingia kumuona kiongozi huyo mkongwe wa siasa za Tanzania.

"Maalim anaendelea vizuri, lakini bado hajaruhusiwa anaendelea kupumzika na kwa leo (jana) hatumruhusu mwandishi yeyote kumuona," alisema Jussa.

Alisema kwa sasa amezuiliwa dawa zote zinazotumia na kwamba tiba yake inahusisha vidonge tu.

Jussa alisema: "Tumeamua kudhibiti watu kumuona kwa sababu, jana (juzi) tuliwaruhusu na Maalim Seif akazungumza nao... sidhani kama kutakuwa na jipya la kumuuliza, alisema.

Alisema hata daktari wake ameridhika na maendeleo ya afya yake na kwamba huenda akamruhusu leo, baada ya kumuangalia.

Jussa ambaye aliteuliwa hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete kuwa mbunge, alisema Maalim Seif anahitaji muda mzuri wa kupumzika ili kurahisisha kuimarika kwa afya yake.

"Kwanza leo (jana) mtamuuliza nini, kama ni kuongea alishaongea kwa kweli kama mnampenda mwacheni apumzike, anahitaji muda huo kwa sasa," alisema Jussa.

Kuugua ghafla kwa Maalim Seif kulisababisha uvumi kuzuka na kuenea kwa kasi jijini Dar es salaam na visiwani Zanzibar zikidai kuwa mkongwe huyo wa siasa amefariki, hali iliyomlazimu aongee na waandishi kukanusha habari hizo.

CHANZO MWANANCHI

Comments
Add New Search
Write comment
Name:
Email:
 
Title:
UBBCode:
[b] [i] [u] [url] [quote] [code] [img] 
 
 
Please input the anti-spam code that you can read in the image.

3.26 Copyright (C) 2008 Compojoom.com / Copyright (C) 2007 Alain Georgette / Copyright (C) 2006 Frantisek Hliva. All rights reserved."

Habari Motomoto

  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
  • 6
  • 7
  • 8
  • 9
  • 10
  • 11
  • 12
  • 13
  • 14
  • 15
  • 16
  • 17
  • 18
  • 19
  • 20

Login Form