Saturday, July 31, 2010
   
Text Size

Tafuta kwenye Website hii

Rufaa ya mgombea binafsi ngoma nzito

Jaji Mkuu wa Tanzania, Augustine Ramadhan, amewaandikia barua maprofesa wawili wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), akiwaomba wawe marafiki wa mahakama katika usikilizwaji wa rufaa ya mgombea binafsi itakayosikilizwa na Mahakama ya Rufaa Aprili 8, mwaka huu.

Maprofesa hao, ambao ni wanasheria kitaaluma na wahadhiri waandamizi, ni Jwan Mwaikusa na Palamagamba Kabudi, ambaye ni Mkuu wa Kitivo cha Sheria cha UDSM.

Katika barua yake ya Machi 3, mwaka huu, Jaji Mkuu amewaomba maprofesa hao kuwa marafiki wa mahakama na wajielekeze katika hoja zao kama mahakama inaweza kutamka kifungu gani cha katiba kinakwenda kinyume cha Katiba.

Aidha, Aprili 8, mwaka huu, Profesa Mwaikusa na Kabudi watachangia hoja kuhusu shauri hilo, litakaposikilizwa na Mahakama ya Rufani, mbele ya jopo la majaji saba linaloongozwa na Jaji Mkuu.

Mahakama hiyo inatarajia kusikiliza rufaa ya serikali dhidi ya uamuzi uliotolewa na waliokuwa majaji wa Mahakama Kuu; aliyekuwa Jaji Kiongozi, Amir Manento, Salum Massati (sasa Jaji wa Mahakama ya Rufaa) na Thomas Mihayo (Mstaafu).

Majaji hao katika hukumu yao, walikubaliana na hoja zilizotolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Democrat (DP), Mchungaji Christopher Mtikila za kuwapo mgombea binafsi katika uchaguzi wa siasa nchini.

Jopo la majaji saba wa Mahakama ya Rufaa, wakiongozwa na Jaji Mkuu, linawajumuisha Jaji Eusebia Munuo, Januari Msofe, Nathalia Kimaro, Mbarouk Salim, Dk. Stephen Bwana na Benard Ruanda, watasikiliza rufaa hiyo.

Katika rufaa yake namba 45 ya mwaka jana, serikali imetoa sababu sita za kukata rufaa hiyo zikiwemo, Mahakama Kuu ilikosea kujipa mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo; ilikosea kutengua vifungu vya Katiba ya nchi; na ilikosea kisheria kwa kupunguza matakwa ya lazima ya Ibara 30 (5) na 13 (2) ya Katiba ya nchi.

Sababu nyingine ni kujipachika mamlaka ya kibunge ya kutunga sheria; kukosea kisheria kwa kuiweka Katiba ya nchi katika vyombo vya kimataifa; na pia ilikosea kuitolea maamuzi kesi hiyo bila kuweka suala hilo bayana.

Mara ya kwanza serikali ilikata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu, katika Mahakama ya Rufaa mwaka 2007, ambapo ilidai mahakama hiyo ya chini ilikosea kisheria kutafsiri Ibara ya 21(1) (c), 39 (1) (c) (b) na 69 (1) (b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Hata hivyo, rufaa hiyo ilitupiliwa mbali na Mahakama ya Rufaa baada ya kukubaliana na ombi la wakili wa Mtikila, Richard Rweyongeza, kwamba rufaa hiyo haina msingi na kwamba imejaa dosari za kisheria.

Awali, katika hukumu ya Mahakama Kuu iliyotolewa Mei 2006, iliruhusu kuwapo kwa mgombea binafsi katika uchaguzi, kwa sababu Katiba ya nchi inatoa haki hiyo.

Mahakama Kuu ilibainisha kuwa katiba inatamka wazi kuwa, kila mwananchi ana haki ya kuchagua au kuchaguliwa kuwa kiongozi na haiweki masharti kuwa hilo lifanyike kwa mtu kujiunga na chama fulani.

Hii ilikuwa mara ya pili kwa Mtikila kupigania mgombe binafsi mahakamani, mwaka 1993 alishinda kesi kama hiyo katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, lakini licha ya uamuzi huo wa mahakama, Bunge lilishindwa kutunga sheria ya kuruhusu mgombea binafsi, hivyo alifungua kesi hiyo ya Kikatiba Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam ambako alishinda tena.

Rufaa hiyo ya serikali ilitajwa Februari 8 na iliahirishwa hadi Aprili 8, mwaka huu, kwa ajili ya kusikilizwa.


CHANZO: NIPASHE
Comments
Add New Search
Write comment
Name:
Email:
 
Title:
UBBCode:
[b] [i] [u] [url] [quote] [code] [img] 
 
 
Please input the anti-spam code that you can read in the image.

3.26 Copyright (C) 2008 Compojoom.com / Copyright (C) 2007 Alain Georgette / Copyright (C) 2006 Frantisek Hliva. All rights reserved."

Habari Motomoto

  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
  • 6
  • 7
  • 8
  • 9
  • 10
  • 11
  • 12
  • 13
  • 14
  • 15
  • 16
  • 17
  • 18
  • 19
  • 20

Login Form